Tuesday, March 22, 2016

Wkb

#KutokaMagazetini - MWANDISHI ALIYETOWEKA, APATIKANA. Siku tatu baada ya mwandishi wa Mwananchi na DW, Salma Said kutoweka, jana alipatikana baada ya kukutwa katika Hospitali ya Regency ya jijini hapa na kupelekwa kituo kikuu cha polisi kuhojiwa. Habari zilizopatikana jana jioni na kuthibitishwa na mumewe, Ali Salim Khamis na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi, Simon Siro zilisema Salma alisajiliwa jana mchana katika hospitali hiyo. Ali aliyekuwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, alisema kwa ufupi kuwa amepata taarifa hizo na kufika Dar es Salaam kuzifuatilia. Kamanda Siro alisema ni kweli Salma amepatikana na ametumwa mkuu wa upelelezi wa kanda hiyo kumfuata hospitali ampeleke kituoni kwa mahojiano. Mpaka tunakwenda mitamboni Salma alikuwa anahojiwa. Awali, wadau wa habari waliungana na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), kueleza hofu yao kutokana na kutoweka kwa mwandishi wa habari, Salma Said na kuvitaka vyombo vya dola kulitafutia ufumbuzi wa haraka suala hilo. Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na MwanaSpoti, Francis Nanai alisema wanaendelea kufuatilia kwa makini suala hilo. “Taarifa za kutoweka kwa Salma zilitufikia Ijumaa mchana Machi 18, 2016 kupitia kwa mume wake, mpaka sasa hakuna taarifa yoyote inayoonyesha ni nani au chombo gani kinamshikilia au kumhifadhi, hali hii inatutia wasiwasi mkubwa kama kampuni na wadau wa habari nchini,” alisema Nanai. Wakati huo huo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika tamko lake ililolitoa jana ilieleza kuwa kutekwa kwa mwanahabari huyo kumezua maswali mengi kwa wananchi, familia yake, wadau na wanahabari wa ndani ya nchi na wale wa jumuia za kimataifa. “Kutekwa kwa Salma kunatokana na kazi yake ya uanahabari, ndiyo maana ushahidi wa awali uliopatikana kwa njia ya ujumbe wa sauti ukiwa na sauti inayoaminika kuwa ni yake, ulieleza wazi kutekwa kwake kunatokana na yeye kuripoti dosari zinazoendelea katika uchaguzi wa marudio Zanzibar,” alisema Joseph Mbilinyi, Waziri Kivuli wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo wa Kambi ya Upinzani. #Mwananchi

No comments:

Post a Comment